Nafasi Ya Matangazo

April 20, 2024

Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Sixtus Mapunda akizungumza na timu ya wataalamu wa mazingira na ustawi wa jamii ya TARURA  na  wilaya ya Temeke



Na Mwandishi Wetu, Temeke
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Sixtus Mapunda ameitaka timu ya wataalamu wa mazingira na ustawi wa jamii ya TARURA  na  wilaya ya Temeke kukaa pamoja na kutengeneza mpango kazi mzuri wa uwasilishwaji wa taarifa za utunzaji wa mazingira katika wilaya yake.

Mhe. Mapunda ameyasema hayo katika kikao cha pamoja baina yake na timu ya TARURA kilichofanyika katika ofisi yake ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya kutekeleza sheria za kutunza na kulinda mazingira kwenye mitaro ya Barabara kwa kushirikiana na wilaya zilizopo mkoa wa Dar es Salaam.

Mhe. Mapunda  ameipongeza TARURA  kwa kazi nzuri wanazofanya katika sekta ya miundombinu ya barabara wilayani Temeke na ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika ulinzi wa Miundombinu hiyo. 

Timu ya wataalamu  kutoka TARURA ikiongozwa na Meneja wa TARURA mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Geofrey Mkinga na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mazingira na Ustawi wa Jamii Bi. Leticia Mapunda  inaendelea kufanya mazungumzo na Wakuu wa Wilaya kwa lengo la kufanya uhamasishaji  kuhusu usimamizi wa sheria ya mazingira zilizo chini ya mamlaka ya Manispaa na Jiji katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Posted by MROKI On Saturday, April 20, 2024 No comments






🔴Imeshika nafasi ya Kumi kwa uzalishaji wa Kinywe Duniani

Na Mwandishi Wetu,Handeni Tanga
Mradi wa Uchimbaji na Uchenjuaji Madini ya Kinywe wa GODMWANGA GEMS LIMITED uliopo katika eneo la Kwamsisi, wilaya ya Handeni Mkoani Tanga  unatajwa kuwa mradi wa kwanza Barani Afrika kwa uchimbaji na uchenjuaji wa Madini hayo na hivyo kushika nafasi ya kumi Duniani.

Hayo yameelezwa na Meneja wa Mradi wa GODMWANGA-B  Henri Joseph wakati akizungumza na timu ya Maafisa Habari kutoka Wizara ya Madini na Wataalamu wa Tume ya Madini.

Akizungumza na timu hiyo, Joseph  amesema mradi huo umekuwa ukifanya vizuri katika uzalishaji wa madini hayo na unatarajiwa kuzalisha tani 800 kwa siku baada ya ujenzi wa kiwanda kipya kukamilika ifikapo Oktoba 2024.

Aidha, Joseph amesema mradi huo umejikita zaidi kwenye uzalishaji wa Madini Mkakati ambapo kwa sasa Dunia inauhitaji mkubwa wa madini hayo yanayotumika kutengeneza betri za magari ya umeme,  betry za simu, oil, grisi, penseli na vizuia joto.

Pia, Joseph ameeleza kuwa, Mgodi huo umefanikiwa kuigusa jamii kwa kuchangia huduma ikiwemo ujenzi wa kituo kikubwa cha Afya chenye thamani ya shilingi Milioni 200, kujenga Madarasa 6 ya shule ya Sekondari Kitumbi, kukarabati jengo la Mahakama na kukarabati barabara ya kuelekea shule ya Sekondari Kwamsisi iliyopo wilayani Handeni mkoa wa Tanga.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa GODMWANGA-A James Minja amesema Kampuni hiyo imefanikiwa kuajiri zaidi ya Wafanyakazi 200 wa kudumu na wafanyakazi 300 wa mkataba kwa lengo la kuinua vijana kiuchumi na kuendeleza uzalishaji wa Madini hayo kwa wingi.

Minja amesema kwa muda mfupi tangu kuanzishwa kwa mradi huo wamefanikiwa kupata soko kubwa la madini hayo katika nchi mbalimbali ikiwemo China na India.

Ameongeza kuwa, mpaka kufikia Oktoba mwaka 2024 kampuni hiyo itakuwa imekamilisha ujenzi unaoendelea wa mradi mkubwa zaidi ya mara kumi ya ulipo sasa ambapo inatarajiwa kuongeza uzalishaji na kupelekea Tanzania kuwa miongoni mwa nchi Tano Duniani zinazo zalisha madini ya Kinywe kwa kiwango kikubwa.

Pamoja na mambo mengine, Minja ameishukuru Serikali na kuomba kusaidiwa kuboreshewa miundombinu pamoja na huduma zingine hususan huduma za upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika.
Posted by MROKI On Saturday, April 20, 2024 No comments
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza na Timu ya mpira wa miguu ya FGA ya mkoani Ruvuma.





Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ameitaka Timu ya mpira wa miguu ya FGA ya mkoani Ruvuma ambayo inashiriki Ligi Daraja la kwanza katika msimu huu wa mwaka 2023/24 iendelee kupambana na kufanya vizuri ili kucheza ligi hiyo msimu ujao.

Mhe.Ndumbaro ametoa kauli hiyo alipokutana na kuzungumza na timu hiyo Aprili 19, 2024 mjini Songea wakati timu hiyo ilipokua ikijiandaa kusafiri kwenda mkoani Mbeya kuikabili timu ya Mbeya City, Aprili 21, 2024.

Amewataka wachezaji wajiamini na kuonesha uwezo wao ili kuisaidia timu kusonga mbele pamoja na kuweka mazingira mazuri ya kujiuza katika soko la ndani na nje.

Aidha, Waziri Dkt. Ndumbaro amewasisitiza wachezaji hao wapambane ili  kupata alama sita muhimu kwenye michezo miwili iliyobaki ambapo mchezo wao wa mwisho utakuwa dhidi ya Ken Gold ya Jijini Mbeya ili wajihakikishie kubaki katika nafasi nzuri katika ligi hiyo.
Posted by MROKI On Saturday, April 20, 2024 No comments

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel John Nchimbi.





🔴Asisitiza uadilifu na uwajibikaji kwa mali za umma

Na Mwandishi wetu, Njombe
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel John Nchimbi, amesema kazi kubwa iliyofanywa na Serikali, chini ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan, ndani ya miaka mitatu, ni nyezo inayobeba ukweli wa kutosha kusambaratisha uongo unaoenezwa na baadhi ya wapinzani wa kisiasa kupitia mikusanyiko yao. 

Amewataka wana-CCM wote kuendelea kujiamini na kutembea kifua mbele wanapozisema, kuzitangaza na kuikumbusha jamii kuhusu kazi za maendeleo na ustawi wa jamii, zinazofanywa na Serikali za CCM ili wananchi waendelee kuuona ukweli, wakitofautisha na uongo unaoenezwa kwa propaganda nyepesi za kisiasa. 

Balozi Nchimbi amesema hayo leo, Aprili 19, 2024, alipokuwa akiwahutubia maelfu ya wanaCCM wa Mkoa wa Njombe, kupitia Mkutano Maalum wa Mkoa, uliofanyika  mjini Njombe.

“Mambo yaliyofanywa na Serikali ndani ya hii miaka mitatu, unaweza kuona kama ni miujiza. Kazi kubwa sana inafanyika. Ni wajibu wetu kuitumia nyenzo yenye ukweli kupambana,” amesema.

Kupitia mkutano huo, ambao Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka aliwasilisha taarifa ya mrejesho wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020 - 2025, iliyohusisha miradi mbalimbali ya maendeleo na ustawi wa wananchi, Balozi Nchimbi pia amerudia kusisitiza kwa watendaji wa Chama na Serikali ulazima na umuhimu wa kuwa waadilifu wakati wote kwenye masuala yanayohusu rasilimali za umma, kwa kupiga vita rushwa na ubadhirifu.
Posted by MROKI On Saturday, April 20, 2024 No comments

April 19, 2024

Waziri Mkuu, Kassim  Majaliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko wakipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Mradi wa Gesi Asilia wa Kampuni ya DIT Limited, Dkt. Esebi Nyari kuhusu matumizi ya gesi asilia badala ya mafuta kwenye magari alipotembelea Maonesho ya Wiki ya Nishati kwenye Viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Aprili 19, 2024
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akipata maelezo kuhusu Nishati Safi ya Kupikia kutoka kwa Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Nishati Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage wakati wa Maonesho ya Wiki ya Nishati  Jijini Dodoma,tarehe 19 Aprili 2024.
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa Maonesho ya Wiki ya Nishati Jijini Dodoma, tarehe 19 Aprili 2024.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza wakati wa Maonesho ya Wiki ya Nishati Jijini Dodoma, tarehe 19 Aprili 2024.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozana na Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Doto Biteko  na Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson baada ya kufunga Maonesho ya Wiki ya Nishati kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Aprili 19, 2024. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko baada ya kufunga Maonesho ya Wiki ya Nishati kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Aprili 19, 2024
.
*******************

🔴Ampongeza Rais Dkt. Samia kwa kutenga sh. trilioni 8.18 sekta ya nishati

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kutenga fedha za kutekeleza miradi ya nishati ambapo katika kipindi cha miaka mitatu zaidi ya shilingi trilioni 8.18 zilitolewa.

 

“Maono na maelekezo yake kuhusu usimamizi wa sekta hii yamekuwa na mchango mkubwa katika ufanisi wa shughuli za sekta, katika hili, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuweka kipaumbele kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya nishati.”

 

“Katika kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa umeme nchini, tayari nchi yetu imeanza kutumia umeme wa bwawa la Julius Nyerere Hydropower Project (JNHPP). Huu ni ushindi na kielelezo tosha kwamba Mama yupo kazini.”

 

Ametoa pongezi hizo leo jioni (Ijumaa, Aprili 19, 2024) wakati akifunga Maonesho ya Wiki ya Nishati yaliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

 

Waziri Mkuu amelipongeza Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kwa kuweza kuzalisha umeme zaidi ya mahitaji yaliyopo sasa. “Leo tarehe 19 Aprili, 2024 uzalishaji wa umeme ni mkubwa. Shirika letu la TAMESCO limemudu kuzalisha umeme zaidi ya mahitaji tuliyonayo na bwawa la Julius Nyerere Hydropower Project limeanza kazi na tayari megawati 235 ziko kwenye mfumo.”

 

Ameitaka Wizara hiyo iweke mkakati wa kuhakikisha maonesho hayo yanakuwa endelevu ili Waheshimiwa Wabunge waweze kupata fursa ya kuwasilisha hoja zao mahsusi na kutatua kero za wananchi wanaowawakilisha.

 

Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya washiriki wa maonesho hayo ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita, Waziri Mkuu ameitaka Wizara hiyo ione uwezekano wa kuandaa maonesho kama hayo katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri. “Wakurugenzi wa Kanda na Mameneja wa Mikoa na Wilaya mko hapa. Nendeni mkae na muangalie jinsi ya kutekeleza jambo hilo,” amesisitiza.

 

Ameitaka Wizara hiyo iweke mkakati wa kuhakikisha wananchi wote wanapata ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu fursa zinazopatikana kutokana na miradi inayotekelezwa na sekta ya nishati. “Pamoja na kuyaleta maonesho hapa Bungeni, kuna haja ya kupeleka maonesha kama haya kwenye maeneo ya katiati ya mji ili muweze kuwafikia wananchi wengi zaidi na kujibu hoja zao,” amesema.

 

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wadau mbalimbali walioshiriki  maonesho hayo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameipongeza TANESCO kwa kuendelea kufanya kazi nzuri ya kuhakikisha wananchi wanapata nishati ya umeme.

 

Naye, Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amesema sekta ya nishati ni kati ya sekta mtambuka kwa sababu inalisha sekta nyingine nyingi na ikitikisika, inatikisa na maeneo mengine pia.

 

Amesema pamoja na utoshelevu wa umeme kwenye gridi ya Taifa, ili kuwe na maendeleo bado nchi inahitaji umeme wa kutosha na hasa kwenye viwanda na siyo kuwasha taa za majumbani.

 

Ameitaka Serikali itafute njia ya kutumia vizuri maji yanayotoka kwenye bwa la JNHPP ili yaweze kuwanufaisha wananchi wanaoishi maeneo ya jirani na bwawa hilo. “Bwawa limejaa kwa hiyo Serikali ihakikishe maeneo ya jirani yanapata maji ya kutumia. Tuanzishe gridi ya maji kama ilivyo kwenye gridi ya umeme. Kule chini tutengeneze njia ya kutunza maji kwa ajili ya matumizi ya umwagiliaji na mifugo,” amesema.

 

Naye, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema ushiriki wa mwaka huu umevunja rekodi kwani watu zaidi ya 480 walitembelea maonesho hayo ambapo 267 walikuwa ni Waheshimiwa Wabunge.

 

Ameyataja maeneo ambayo washiriki walikuwa wakiulizia zaidi ni umeme, nishati ya jua, nishati jadidifu, nishati safi ya kupikia, mafuta na gesi.

 

Amesema ili kujenga uelewa mpana kwa wananchi, wanapanga kuandaa kongamano maalum juu ya gesi asilia ambalo linatarjiwa kufanyika Mei, mwaka huu.

Posted by MROKI On Friday, April 19, 2024 No comments
Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego









Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego amepiga marufuku wananchi wa mkoa huo kuanza kunywa pombe asubuhi badala ya kufanya shughuli za maendeleo na za kiuchumi hali ambayo inaweza kusababisha kudumaa kwa shughuli za kiuchumi kwa wananchi hao na Taifa kwa ujumla.

Mkuu wa mkoa huyo ametoa kauli hiyo katika Kijiji cha Kashangu, Halmashauri ya ITIGI kwenye ziara yake ya kikazi ya Siku Mbili ya kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo ya Elimu na Afya.

HALIMA DENGEGO ameonya kuwa hatasita kuwachukulia hatua Viongozi wa Vijiji na kata ambao watashindwa kudhibiti hali hiyo ya unywaji wa pombe nyakati za asubuhi badala ya kuhimiza wananchi kwenda kufanya shughuli halali za kijitafutia riziki.

“Mnaanza kunywa Pombe asubuhi hasa watoto wa kike hii Sio sawa lazima tusimamiane nikikuta jambo linaenda ndivyo sivyo nitakamata Mtendaji kwa sababu anasheria kama zangu na kwanini ashindwe kudhibiti vitendo hivyo tutawajibishana vikali,” Amesisitiza Halima Dendego.

Kuhusu utoaji wa chakula mashuleni, Mkuu wa mkoa wa SINGIDA amewaagiza Wakuu wa Shule zote za mkoa wa SINGIDA kwa ushirikiano na Viongozi wa Vijiji na kata kuweka utaratibu wa kutoa chakula kwa wanafunzi ili kuhakikisha wanajifunza kwa bidii.

Amesema utoaji wa chakula mashuleni utasaidia kwa kiasi kikubwa kupandisha ufauli kwa wanafunzi hivyo ni muhimu kwa kila shule kuanza utaratibu wa kutoa chakula kwa wanafunzi wao.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt Fatma Mganga amewataka Watendaji wa Halmashauri na Kata mkoani humo kusimamia vizuri ujenzi wa miradi ya maendeleo hasa umaliziaji wa majengo mbalimbali ili kudhibiti vitendo vya wizi wa vifaa vya ujenzi.

Amesema hatapenda kusikia wala kuona wizi wa vifaa katika miradi ya maendeleo hivyo Viongozi lazima wasimamie kikamilifu utekelezaji wa miradi hiyo ili iweze kuleta manufaa kwa Wananchi na sio vinginevyo.

Katibu Tawala huyo amesema kumekuwa na tabia kuiba vifaa hasa vinapopelekwa kwenye miradi ya maendeleo jambo ambalo linasababisha utekelezaji wa baadhi ya miradi kujengwa chini ya kiwango na kusisitiza kuwa tabia hiyo itakoma iwapo Viongozi wote watashirikiana katika ngazi zote.
Posted by MROKI On Friday, April 19, 2024 No comments
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela  alipokwenda  nyumbani kwa Mheshimiwa Malecela eneo la Uzunguni jijini Dodoma kumtakia heri  ya kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa, Aprili 19, 2024. Kulia ni mke wa Mzee Malecela Ambaye pia ni Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela. (
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela zawadi ya kikombe  alipokwenda nyumbani kwa Mheshimiwa Malecela eneo la Uzunguni jijini Dodoma kumtakia heri   ya kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa , Aprili 19, 2024. Katikati ni mke wa Mzee Malecela Ambaye pia ni Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela zawadi  alipokwenda nyumbani kwa Mheshimiwa Malecela eneo la Uzunguni  jijini Dodoma kumtakia heri   ya kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa, Aprili 19, 2024.Katikati ni mke wa Mzee Malecela Ambaye pia ni Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Posted by MROKI On Friday, April 19, 2024 No comments
WAZIRI MKUU Kasim Majaliwa amesema bila uhuru, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hawezi kutimiza ipasavyo wajibu wake wa kuhakikisha uwazi na uwajibikaji vinakuwepo katika matumizi ya fedha za Serikali.

Amesema nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) zinapaswa kutambua maeneo yanayostahili kutiliwa mkazo baina ya Serikali, Bunge, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi za Ukaguzi na Mabunge kwenye nchi za SADC (SADCOPAC).

Amesema miongoni mwa maeneo hayo ni kuunga mkono uhuru wa Ofisi ya CAG. “Bila uhuru, CAG hawezi kutimiza wajibu wake ipasavyo katika kuhakikisha uwazi na uwajibikaji wa fedha za Serikali. Kwa hiyo wadau wote wanawajibika kulinda uhuru huu kupitia hatua za kisheria na msaada wa taasisi zenu,” amesema.

Alitoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Aprili 18, 2024) wakati akifunga Mkutano wa Kujenga Uelewa wa Pamoja na Ufanyaji wa Kazi wa Taasisi za Ukaguzi na Mabunge kwenye nchi za SADC (SADCOPAC) uliofanyika kwa siku mbili kwenye hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar.

Alisisitiza kuwa suala la kuimarisha uhusiano kati ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (AG) na Bunge ni la muhimu kwani linasaidia kurahisha utendaji kazi baina yao. “Ushirikiano kati ya vyombo hivi unawezesha utendaji na usimamizi rahisi, unaruhusu uchunguzi mzuri zaidi wa matumizi ya fedha za serikali. Ushirikiano huu unaweza pia kuboresha utawala na uwajibikaji ndani ya nchi wanachama,” alisema. 

Aliwataka washiriki wa mkutano huo waweke kipaumbele katika kuboresha utawala bora na uwajibikaji kwenye nchi zao. “Kupitia hatua za kisheria na usimamizi, tunapaswa  tuhakikishe kuwa mifumo iko sawa na inaweza kuziwajibisha taasisi za Serikali kupitia  matumizi yao. Kwa kuzingatia haya, tunaweza kukuza uaminifu kwenye mifumo yetu ya utawala na ustawi wa raia wetu,” alisisitiza. 

Katika kusisitiza ushirikiano wa kikanda, Waziri Mkuu aliwaambia washiriki wa mkutano huo kwamba ushirikiano baina ya SADCOPAC na washirika wa kikanda unapaswa kuendelezwa na kuwaahidi kuwa Tanzania ikiwemo Zanzibar imejipanga kikamilifu kufanya kazi bega kwa bega na washirika hao ili kuboresha shughuli za ukaguzi kwenye ukanda huo.

“Serikali imejitolea kusaidia Taasisi Kuu za Ukaguzi (Supreme Audit Institutions), Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali (PACs) na wadau wengine muhimu ili kuhakikisha kunakuwa na matumizi bora na ya uwazi ya rasilimali za umma, njia ambayo inakuza utawala bora.”

Mapema, kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar, Mudrik Ramadhani Soraga alisema Tanzania imefaidika kiuchumi na kimkakati kutokana na mkutano huo kufanyika nchini.

"Wabunge na wawakilishi waliokutana hapa wamejadili mada ambazo zitawawezesha kusaidia Serikali zao katika nchi za SADC kuimarisha uwajibikaji na matumizi mazuri ya rasilimali na mapambano dhidi ya rushwa. Lakini nikiwa Waziri mwenye dhamana ya utalii, mkutano huu umetuongezea mapato,” alisema Soraga.

Naye, Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Dk Othman Abbasi Ali ambaye ofisi yake ilikuwa mwenyeji wa mkutano huo, alisema mbali na kuimarisha ushirikiano, mkutano wa SADCOPAC umetoa fursa kwa wajumbe wa PAC katika mabunge kubadilishana uzoefu wa njia bora za kufuatilia matumizi bora ya fedha za Serikali kwenye nchi zao.

Naye, Mbunge kutoka Malawi na Mweka Hazina wa SADCOPAC, Mark Botomani, aliwashukuru Marais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuweka mazingira mazuri yaliyowezesha mkutano huo kufanyika kwa usalama na kwamba Tanzania imekuwa mshirika muhimu wa Jumuiya ya SADC.

Kwa niaba ya wajumbe wenzake wa SADCOPAC, Botomani ameahidi kuwa watafanyia kazi mambo yote waliyojifunza kwenye mkutano huo wa siku mbili ambao awali ulifunguliwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Mwinyi. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na taasisi za ukaguzi kutoka nchi za SADC.

Posted by MROKI On Friday, April 19, 2024 No comments




Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde leo Aprili 19, 2024 amefanya kikao cha pamoja na  Kampuni ya Perseus ya Australia ikiongozwa na Mtendaji Mkuu wake *Bw. Jaffer Quartamaine* kilichojadili kuhusu uendelezwaji wa mradi wa uchimbaji madini ya dhahabu wa Nyanzaga unaomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Ore Corp ambayo hisa zake zimenunuliwa na Kampuni ya Perseus.

Katika Mkutano huo, Waziri Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa kufanikiwa kukamilisha wa mchakato wa ununuzi wa hisa za Kampuni ya Ore Corp na kuitaka Kampuni hiyo kukamilisha kwa uharaka malipo ya fidia kwa wananchi wanaopisha mradi.

Pia, Waziri Mavunde amewataka wawekezaji hao kuhakikisha wanaanza mapema uendelezaji wa mradi kwa mujibu ya makubaliano ya awali ya kimkataba ili nchi ianze kunufaika na matunda ya utekelezaji wa mradi huu mkubwa wa dhahabu katika Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa Mwanza.

Akizungumza katika kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Perseus *Bw. Jaffer Quartamaine* ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa wakati wote wa mchakato wa ununuzi wa hisa za Kampuni ya Ore Corp na kuahidi kwamba wamejipanga kuanza uendelezaji wa mradi huu mapema kadri iwezekanavyo kutokana na mpangilio wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za utekelezaji wa mradi.

Ameongeza  kwamba, kampuni hiyo imejipanga kufanya uwekezaji mkubwa na wa mfano kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kuongeza uzalishaji wa dhahabu nchini.
Posted by MROKI On Friday, April 19, 2024 No comments
  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo